Ujasiriamali huchangia mno ukuaji wa kiuchumi: UNCTAD

6 Mei 2013

Kuanzisha biashara mpya, husan zile ndogondogo na zile za ukubwa wastani (SMEs) ni chanzo cha kuchagiza ukuaji na ustawi wa ukichumi, na kuchangia pakubwa katika ubunifu na kuongeza nafasi za kazi, wamesema wataalam katika mkutano wa ngazi ya juu wa Tume ya Uwekezaji, Ujasiriamali na Maendeleo.

Katika mkutano wa mawaziri na maafisa wa ngazi ya juu wa serikali ulioangazia ujasiriamali, wataalam hao wamesema kuwa ikiwa nchi maskini zitataka kuiga chumi zilizoendelea, ni lazima ziendeleze ustadi katika ujasiriamali na kuendeleza biashara ndogondogo na za wastani, ambazo ndizo hutoa nafasi nyingi zaidi za ajira na kuongeza uzalishaji kwa ujumla katika nchi zilizoendelea kiuchumi.

James Zhan ambaye ni Mkurugenzi wa kitengo cha Uwekezaji na Ujasiriamali katika Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo, UNCTAD, amesema biashara ndogondogo na za wastani zilichangia kwa kiasi kikubwa kwa chumi za kitaifa na utajiri wa kimataifa, na kuchangia thuluthi mbili za nafasi za ajira, pamoja na nusu ya mapato katika nchi zilizoendelea, huku zikichangia asilimia 40 ya nafasi za ajira na asilimia 25 ya mapato katika nchi zinazoendelea.