Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vikwazo vya kiurasimu huko Syria viondolewe: Baraza la Usalama

Vikwazo vya kiurasimu huko Syria viondolewe: Baraza la Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetaka vikwazo vyote vile vya kiurasimu vinavyokwamisha upelekaji wa misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa Syria walionaswa katika mzozo wa kivita ndani ya nchi yao viondolewe. 

Rais wa baraza hilo Balozi Eugène-Richard Gasana ametoa tamko hilo la baada ya kikao cha mashauriano kuhusu Syria ambapo maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa akiwemo Mkuu wa shirika la kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Valerie Amos alisema wanakatishwa tamaa kwa kuwa licha ya hali mbaya ya usalama kwa wafanyakazi wao, bado kuna vikwazo vingi ambavyo magari yenye shehena ya misaada yanavipitia kabla ya kufika eneo husika ikiwemo Allepo.

 (SAUTI YA GASANA)

"Wajumbe wa baraza la usalama wanasihi pande zote nchini Syria kuhakikisha mashirika ya misaada yanafikia wenye mahitaji kwa usalama na bila vikwazo vyovyote. Wamechukizwa na vikwazo wakati wa utoaji wa misaada ya kibinadamu na wamesisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo vyote vya aina hiyo ikiwemo vile vya kiurasimu.”

Wajumbe hao pia wametaka pande pinzani nchini Syria kusitisha mapigano na kuweka fursa ya mchakato wa kisiasa kwa mujibu wa tamko la pamoja la Geneva la mwezi Juni mwaka jana.