MONUSCO yahifadhi wakimbizi waliokimbia mapigano Kitchanga

1 Aprili 2013

Walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wamesaidia kuwapatia hifadhi wakimbizi wa ndani wapatao 1,500 waliokimbia kufuatia mapigano mapya kati ya majeshi ya serikali na vikundi vyenye silaha huko Kitchanga, Mashariki mwa nch hiyo.

Eduardo del Buey kutoka ofisi ya msemaji wa Umoja wa Mataifa amekariri ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO ukieleza kuwa katika mapigano hayo askari mmoja wa kikosi cha serikali FARDC alijeruhiwa huku wapiganaji 11 wa kikundi cha waasi cha APCLS wakiuawa.

Hata hivyo hali sasa imetulia na MONUSCO inaendelea kufuatia hali halisi na kufanya doria kwenye eneo hilo.

Mapigano hayo yameibuka siku chache tu baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuipatia MONUSCO mamlaka mpya ikiwemo kuwa na brigedi ambayo itajibu mashambulizi pindi vikundi vya waasi Mashariki mwa DRC vitakapofanya mashambulizi yanayohatarisha usalama.