Baraza la Usalama kupitisha azimio kuhusu DRC

28 Machi 2013

Baraza la Usalama baadaye leo linatarajiwa kupiga kura juu ya rasimu ya azimio iliyowasilishwa na Ufaransa kuhusu shughuli za ulinzi wa amani huko Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Mapendekezo hayo yanazingatia ripoti ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu DRC na nchi za Maziwa Makuu ambayo pamoja na mambo mengine imependekeza kuangaliwa upya kwa mamlaka ya ujumbe wa Umoja huo nchini DRC, MONUSCO.

Ripoti hiyo inataka kuzingatiwa kwa vipaumbele sita katika kupanga upya mamlaka ya ofisi hiyo ambapo vipaumbele hivyo ni pamoja na mchakato wa kisiasa unaojumuisha wadau wote nchini DRC, upokonyaji silaha na ujumuishaji wa vikundi vyote katika jamii na kusaidia kuanzisha mfumo wa kitaifa wa kudhibiti uchimbaji madini Mashariki mwa DRC kwa maslahi ya Taifa.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter