Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo wa Syria wachangia ongezeko la watu wanaoomba hifadhi salama nchi zilizoendelea: UNHCR

Mzozo wa Syria wachangia ongezeko la watu wanaoomba hifadhi salama nchi zilizoendelea: UNHCR

Ripoti mpya ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, UNHCR, imesema mizozo mipya na ile ya zamani mwaka uliopita, ikiwemo ile ya Syria, Afghanistan, Iraq, na Somalia imechangia kuongezeka kwa idadi ya watu wanaoomba hifadhi salama katika nchi zilizoendelea kwa asilimia 8 zaidi mnamo mwaka 2012. Ripoti inasema ongezeko kubwa zaidi lilishuhudiwa katika raia wa Syria wanaofanya maombi hayo.

Kwa mujibu wa Shirika la UNHCR, maombi takriban 480, 000 yalisajiliwa katika nchi 44, ambazo zimefuatiliwa katika ripoti ya UNHCR kuhusu mienendo ya maombi ya hifadhi salama mwaka 2012, na ambayo imetolewa leo.

Idadi hiyo ndiyo kubwa zaidi tangu mwaka 2003, ikionyesha mwenendo unaoongezeka kila baada ya mwaka mmoja tangu mwaka 2006. Kamishna Mkuu wa UNHCR, Antonia Guterres amesema vita vinawalazimu watu kuomba hifadhi, na hivyo kufanya haja ya kuimarisha mfumo wa kimataifa kuhusu hifadhi kuwa muhimu hata zaidi.

Guterres ametoa wito kwa nchi zifungue mipaka yao kwa watu wanaokimbilia uhai wao. Nchi ya Marekani ndiyo ilowapokea wakimbizi wengi zaidi wanaoomba hifadhi, wakiwa zaidi ya 80, 000.