Hatua za kibinadamu ni za kipaumbele katika majukumu yetu Afghanistan: Ban

19 Machi 2013

Wakati taifa la Afghanistan likijiandaa kwa kipindi cha mpito, Umoja wa Mataifa utatakiwa kuchukua hatua za kibinadamu ili kukabiliana na hatari zinazolikabili taifa hilo, na hali inayotokana na kipindi cha mpito. Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, katika hotuba yake kwa Baraza la Usalama hii leo.

Akizungumza kuhusu majukumu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA, Bwana Ban amesema Umoja wa Mataifa unatakiwa kuendeleza kazi ya kutafuta maridhiano na ushirikiano wa kikanda, na kuimarisha msimamo wake wa kuetetea haki za binadamu, na kuchagiza maendeleo.

Ametoa wito kwa raia wa Afghanistan kushirikiana, sio tu katika kumaliza migogoro, bali pia kuchukua uongozi na kudhibiti harakati za kipindi cha mpito kwa ajili ya taifa lao.

Katika mkutano huo, Baraza la Usalama limepitisha azimio la kuongeza muda wa ujumbe wa UNAMA kwa mwaka mmoja zaidi.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud