Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kubuni ajenda ya maendeleo endelevu ni kubuni ushirikiano endelevu: Jeremic

Kubuni ajenda ya maendeleo endelevu ni kubuni ushirikiano endelevu: Jeremic

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Vuk Jeremic, amesema harakati za kubuni malengo ya maendeleo endelevu zitakuwa ngumu, na zitahitaji ustadi mkubwa wa kidiplomasia. Bwana Jeremic amesema hayo wakati wa kufungua kikao cha kwanza cha kundi la Baraza Kuu la kuchukua hatua kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu, (SDGs).

Rais huyo wa Baraza Kuu ameongeza kuwa kwa mtazamo wake, kubuni ajenda ya baada ya mwaka 2015 ni sawa na kubuni ushirikiano mpya wa kimataifa ambapo hakuna taifa linaloachwa nyuma, au kujiondoa kwenye ushirikiano huo. Hata hivyo, amesema kutimiza Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) ndio kwanza utakuwa msingi.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya mkutano wa kimataifa wa Rio +20, kundi hilo litahitajika kuwasilisha mapendekezo ya orodha ya malengo ya maendeleo endelevu katika kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Ifikapo robo ya tatu ya mwaka 2014, nchi wanachama zitatakiwa kuwa kutangaza Malengo ya Maendeleo Endelevu, ambayo yataongoza ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, yanapotarajiwa kutimizwa Malengo la ya Maendeleo ya Milenia.