Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lugha ndogo za asili hatarini kutoweka: Mtaalamu UM

Lugha ndogo za asili hatarini kutoweka: Mtaalamu UM

Kikao cha Baraza la Haki za Binadamu kinachoendelea mjini Geneva, Uswisi kimeelezwa kuwa lugha takribani nusu ya lugha Elfu Sita za makabila madogo duniani ziko hatarini kutoweka mwishoni mwa karne hii kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo sera za kitaifa, muingiliano wa jamii na migogoro ya kivita.

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa juu ya masuala ya makundi madogo, Rita Izsák ameonya kuwa hatua stahili zichukuliwe haraka kulinda jamii ndogo na urithi wa lugha zao.

Ametoa mfano kuwa sera za kuwa na lugha rasmi ya taifa kama njia mojawapo ya kukuza utaifa na umoja zimekuwa zikisababisha kutokomea kwa lugha za asili za makabila madogo.

Bi. Izsák amesema haki ya matumizi ya lugha za makabila madogo imekuwa mara kwa mara chanzo cha mvutano kati na baina ya mataifa.

Mtaalamu huyo amesema ili kujenga umoja ndani ya jamii yenye watu wa asili tofauti ni lazima kuwepo na mchakato wa wadau wote wa jinsi ya kujumuisha mahitaji na haki ya lugha ya makundi yote kwani matumizi ya lugha asili ni haki ya msingi na humtambulisha mtu alikotoka.