Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Vikosi vya Ulinzi Amani vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) vimeripotiwa wiki hii kugawa misaada ya chakula kwenye kambi ya wahamiaji wa ndani ya Dereige, msaada ambao utawahudumia chakula fungu kubwa la wahamiaji muhitaji wa kike na watoto wadogo waliopo kambini humo. Vikosi vyaUNAMID pia viligawa vifaa vya ilimu vitakavyotumiwa na watoto mayatima wa kambi hiyo. Hali ya usalama katika Darfur, kwa ujumla, inaripotiwa sasa kuwa ni ya shwari.

Alkhamisi ya tarehe 09 Julai (2009) itaadhimishwa kama ni siku ya ukumbusho wa miaka mitano tangu Mahakama Kuu ya Kimataifa (ICJ) kutoa Ushauri wa Maoni ya kuharamisha uamuzi wa Israel kujenga Ukuta kwenye Eneo la WaFalastina Liliokaliwa Kimabavu (OPT), kitendo ambacho Mahakama ilithibitisha kinatengua majukumu ya Israel chini ya sheria ya kimataifa. Kitengo cha Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu katika eneo la WaFalastina la Ufukwe wa Magharibi ya Mto Jordan, imeripoti hali huko bado haikutengenea tangu Mahakama Kuu ya Kimataifa kutoa maamuzi yake. Ofisi hii ya UM imetoa mwito wenye kuitaka Israel kutekeleza mapendekezo ya Ushauri wa Maoni ya Mahakama ya ICJ, na kubomoa Ukuta haramu uliojengwa kwa kupitia ndani ya Eneo la OPT, na kutakiwa ifidie uharibifu na usumbufu ulioathiri umma baada ya Ukuta huo kujengwa.

Shirika la UM Linalofarajia Huduma za Kiutu kwa Wahamiaji wa KiFalastina wa Mashariki ya Karibu (UNRWA) limeripoti kwamba hii leo Karen AbuZayd, aliye Kamishna Mkuu wa UNRWA aliwakaribisha kwenye ofisi yake vijana wa KiFalastina wa Tarafa ya Ghaza ambao karibuni walirejea nchini kutoka ziara ya mapumziko ya wiki tatu katika Poland, ziara iliotayarishwa na Serikali ya Poland kwa madhumuni ya kuwasaidia hasa wale watoto walioathirika kihali na kiakili na mashambulizi na uvamizi dhidi ya Ghaza uliofanyika mapema mwaka huu na mwisho wa 2008.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imetangaza mashambulio bado yanaendelezwa katika vijiji na miji ya Kivu Kaskazini, yanayoongozwa na wafuasi waasi wa lile kundi la FDLR. Waasi hawa wamegunduliwa wakitenda makosa maovu ya kunajisi kimabavu watu, kuchoma moto kihorera nyumba za raia na kuiba mali za watu pamoja na kuwalazimisha wanavijiji kuwatumikia kwa nguvu, hasa katika zile sehemu za Lubero, Masisi na Walikale.  OCHA imeeleza pia baina ya Januari mpaka Juni 2009 watu 400,000 wa eneo walilazimika kuhama makazi yao katika Lubero Kusini, na katika baadhi ya sehemu za Masisi na Walikale, kwa sababu ya kupamba mapigano makali baina ya vikosi vya Serikali na waasi wa FDLR.

Matokeo ya muda ya tathmini ya pamoja juu ya hali ya chakula nchini Zimbabwe iliofanyika mwezi Mei na mashirika ya UM pamoja na Serikali ya Zimbabwe, imeonyesha kuwepo upungufu wa tani za metriki 670,000 za nafaka nchini kwa mwaka huu. Mashirika ya UM yaliojumuika kuendeleza utafiti yalikuwemo lile shirika linalohusika na miradi ya chakula, WFP, na lile linalozingatia sera za chakula na kilimo, WFP. Watu milioni 2.8 wanaoishi kwenye miji na vijiji wanakabiliwa na hatari ya njaa kwenye majira ya mavuno ya 2009-2010.