Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Haki za binadamu lajadili raia kuwekwa vizuizini ovyo na mapambano dhidi ya ugaidi

Baraza la Haki za binadamu lajadili raia kuwekwa vizuizini ovyo na mapambano dhidi ya ugaidi

Baraza la Haki za Binadamu limekuwa na majadiliano  muhimu na Mads Andenas kutoka kundi la kuchukua hatua kuhusu haki za kuwekwa vizuizini ovyo, na Ben Emmerson, ambaye ni mataalamu maalum wa kutetea na kulinda haki za binadamu katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Katika majadiliano kuhusu haki za kuwekwa kizuizini, wanenaji wamesema mfululizo wa matukio ya raia kuwekwa vizuizini umeongeza umuhimu wa kundi hilo linaloangazia haki za raia hao, huku wengine wakisema licha ya kukithiri kwa vitendo vya raia wengi kuwekwa kizuizini kugusa ulimwengu, tabia ya baadhi ya serikali kuficha ukweli imekuwa ni tatizo kubwa zaidi.

Kuhusu kulinda haki za bianadamu wakati wa kushughulikia maswala ya ugaidi, wanenaji wamelaani vitendo vyote vya ugaidi huku pia wakitaka haki za binadamu kuzingatiwa muda wote wakati wa kushughulikia aina hiyo ya uhalifu. Wanenaji wengine katika majadiliano hayo wamesema swala la vizuizi vya siri linapaswa kushughulikiwa na Baraza na kwamba maswala yote ya kushughulikia ugaidi lazima yafanywe kwa kufuata misingi ya sheria za mikataifa.

Wamesisitiza haki za washukiwa wanaofikishwa mahakamani ili sheria ifuatwe na kuepuka vigezo holela katika mchakato huo.