Skip to main content

UM na washirika wasaidia raia waliokimbia ghasia Darfur

UM na washirika wasaidia raia waliokimbia ghasia Darfur

Umoja wa Mataifa na washirika wake huko Sudan umelazimika kutoa misaada ya dharura na hata kuwasafirisha kwa ndege wahanga wa ghasia mpya za  wiki iliyopita huko jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan.

Ujumbe wa pamoja wa Umoja huo na Umoja wa Afrika huko Darfur, UNAMID umeeleza kuwa mapigano hayo  yametokea wakati ambapo tayari Watu Elfu Sitini kwenye eneo hilo la Magharibi mwa Jimbo la Darfur Kaskazini ni wakimbizi wa ndani kutokana na mapigano ya udhibiti wa machimbo ya dhahabu.

UNAMID imesema mapigano hayo ya wiki iliyipota yalikuwa ni kati ya koo za Abbala na Beni Hussein kwenye eneo la Aji Heir, takribani kilometa 10 kutoka eneo la El Sireaf wanakoishi wakimbizi wa ndani.

Mwakilishi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Ali Al-Za’tari amesema kipaumbele chao kwa sasa ni kuhakikisha usalama wa raia kwenye eneo hilo na kutoa msaada wowote wa kibinadamu unaohitajika.

Umoja wa Mataifa na washirika wake mwezi uliopita iliwapatia wakazi wa eneo hilo tani 700 za ujazo za misaada na kwa mujibu wa Al-Za’tari hofu ya sasa inadhihirisha hatari ambamo raia wanaishi.

Tayari UNAMID imetaka pande husika kwa mvutano huo kuacha mapigano hayo ya kikabila.