Ban akutana na viongozi wa UAE Dubai na Abu Dhabi

25 Februari 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Sheikh Mohammad bin Rashed Al Maktoum, ambaye ni Waziri Mkuu wa ufalme wa United Arab Emirates, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje, Dr. Mohammad Gargash.

Katika mkutano huo, wamezungumza kuhusu maendeleo katika kanda nzima, yakiwemo masuala kuhusu Syria, Iran, Lebanon, Misri na Jordan, pamoja na harakati za amani ya Mashariki ya Kati. Bwana Ban ameishukuru United Arab Emirates kwa mchango wake katika kuunga mkono kazi ya Umoja wa Mataifa, akielezea matumaini yake kuwa itaendelea kuchangia shughuli za kibinadamu za Umoja wa Mataifa na zile za kulinda amani.

Akiwa Dubai, Bwana Ban pia amekutana na Binti Malkia Haya Bint Al-Hussein, ambaye amemshukuru kwa kazi yake ya kibinadamu, na kwa majukumu yake kama mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa. Wamezungumza kuhusu malengo ya maendeleo ya milenia, kampeni ya kutokomeza njaa, pamoja na mzozo wa Syria na athari zake kwa nchi jirani.

Mjini Abu Dhabi, Bwana Ban amekutana na Dr. Sultan Al Jaber, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Masdar, ambayo inaendeleza mazingira safi katika biashara ya nishati.