Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tetemeko la ardhi huko Solomon laacha watu 3500 bila makazi

Tetemeko la ardhi huko Solomon laacha watu 3500 bila makazi

Zaidi ya nyumba 430 zimeharibiwa kwenye mkoa wa Temotu na kuwaacha watu 3500 bila makazi kufuatia tetemeko la ardhi na mawimbi ya baharini, Tsunami vilivyokumba visiwa vya Solomon.

Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka lakini tayari watu sita wameripotiwa kufa huku wengine wanne wakiwa hawajulikani walipo akiwemo mtoto aliyesombwa na maji hadi baharini.

Kituo cha kushughulikia masuala ya dharura kinasema kuwa hakina taswira kamili ya kiwango cha uharibifu vilivyotokea tetemeko hilo la tarehe 6 mwezi huu kwa sababu ya ugumu wa kufikia maeneo yaliyoathirika.

Kando na uharibifu ulioshuhudiwa kwenye visiwa vya Solomon , mawimbi ya tsunami pia yaliripotiwa eneo la Vanuatu karibu na Caledonia na Japan.

Kituo cha masauala ya dharura kimetambua maeneo yanayoweza kutumiwa kama makazi ya dharura yakiwemo makanisa na shule.

Kwa upande mwingine Shirika la msalaba mwekundu kwenye visiwa vya Solomon linafanya jitihada kuweka makazi ya muda kwa waathiriwa wa mkasa huo.