Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uvutaji sigara waongezeka nchi maskini: WHO

Uvutaji sigara waongezeka nchi maskini: WHO

Wakati shirika la afya duniani, WHO likiwa katika maandalizi ya mwisho ya shughuli ya kuanza kutia saini mkataba wa kimataifa wa kutokomeza biashara haramu ya bidhaa zitokanazo na tumbaku siku ya Alhamisi, shirika hilo limesema kwa sasa kuna taswira tofauti ya kiwango cha uvutaji sigara duniani.

Mkuu wa sekretarieti ya mkataba huo Dokta Dr. Haik Nikogosian amewaeleza waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kuwa kwa nchi zinazoendelea bado kiwango kinaongezeka ilhali kuna nchi ambako kiwango kimepungua kutokana na kuongezeka sheria kali za kudhibiti uvutaji bidhaa za tumbaku.

(SAUTI Dkt. Nikogosian)

Matumizi ya tumbaku kwa ujumla duniani kwa bahati mbaya bado hayapungui, kwa sababu matumizi yanapungua kwa baadhi ya nchi hususan zile zilizoendelea ambako kuna sheria kali dhidi ya uvutaji, lakini kuna nchi ambako bado uvutaji unaongezeka. Lakini ukiangalia kwa ujumla kwa kuwa uvutaji sasa umejikita zaidi katika nchi zinazoendelea kwenye jamii maskini, kiwango cha wavutaji kinaongezeka kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu. Lakini hatuwezi kusema kuwa kiwango cha matumizi ya tumbaku duniani kinaongezeka.”