Wakimbizi wapatiwa misaada huko Kivu Kaskazini

7 Januari 2013

Baada ya ghasia kushamiri huko jimbo la Kivu Kaskazini na kusababisah watu kukimbia makwao na hata mashirika ya misaada kushindwa kusambaza huduma za dharura kwa wananchi, hatimaye kazi ya usambazaji imeanza baada ya kuwepo kwa utulivu siku za karibuni. Misaada inayotolewa ni ya kibinadamu. Assumpta Massoi ameandaa ripoti kamili. (SAUTI YA ASSUMPTA)

Msururu mrefu wa wanawake, wanaume na watoto katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Bulengo huko jimbo la Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhri ya Kidemokrasi ya Congo. Idadi hapa ya wakimbizi imeongezeka kutokana na kuongezeka kwa ghasia mashariki mwa DRC na inakisiwa watu Laki Moja na Elfu Thelathini wamekimbia makazi hayo na kuja hapa.

Msururu huo ni wa kupokea misaada ya dharura ambayo imeweza kusambazwa kutokana na utulivu kiasi katika eneo hilo kwa sasa.

Miongoni mwao ni Febe Bushu mwenye umri wa miaka Sitini na Minne akiwa na binti zake wawili na mjukuu mmoja. Wao walitembea kwa takribani wiki mbili kabla ya kufika Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

(SAUTI YA FEBE BUSHU-1- Kiswahilil)

Wakimbizi wa ndani hukumbwa na masahibu mengi kadri mzozo na mapigano yanavyosonga katika makazi yao ya hifadhi a misaada inapopungua.

Kisanga hicho kiliwakumba pia Febe na familia yake baada ya kufika Goma kwani aliyewapatia hifadhi alishindwa kuwapatia misaada.

(SAUTI YA FEBE BUSHU)

Miongoni mwa changamoto kubwa kwa familia za wakimbizi ni kupata chakula cha kujitosheleza yeye na kulisha familia. Msimu wa mvua wa sasa na kweli kwamba mkimbizi hukimbia bila kuchukua kifaa chochote au vifaa vichache vinaongeza machungu ya kuishi ukimbizini. Ulrich Wagner ni afisa kutoka UNICEF.

(WAGNER)

"Tuko kwenye kipindi cha mvua, vile unavyoona sasa kuna mawingu mengi, kwa hivyo imenyesha leo itanyesha usiku watu wanahitaji makao hasa watoto ambao wanaweza kupata maambukizi.

Kuzorota kwa usalama, mashambulizi kutoka kwa waasi na hata vitendo vya uporaji vilikwamisha jitihada za awali za kusambaza misaada kwa wakimbizi.

Hata hivyo kupungua kwa ghasia kwa siku za karibuni huko Kivu Kaskazini kumewezesha shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na washirika wake kusambaza vifurushi vyenye vifaa vya misaada. Vifaa hivyo ni pamoja na mahema, makaratasi ya nailoni, mablanketi, nguo, vifaa vya jikoni na vile vya kuteka maji.

Tariq Riebl ni mratibu wa misaada ya kibinadamu kutoka OXFAM.

"Oxfam ni sehemu ya wakala wa usambazaji wa vifaa visivyo vyakula, NFI inayoratibiwa kimsingi na UNICEF. Tunapatia kila kaya kifurushi chenye bidhaa muhimu kama vile mablanketi, mahema, vifaa vya kupikia, vitu vya aina hiyo vinavyohitajika ili kaya iweze kujitosheleza kwa mahitaji muhimu.”

Usambazaji huo unafanyika kwa ushirika wa mashirika 13 yasiyo ya kiserikali kwenye eneo hilo na ya kigeni pamoja na mashirika manne ya Umoja wa Mataifa. Febe anazungumzia vile misaada hiyo itakavyomsaidia.

(SAUTI YA FEBE-3- Kiswahili)

Bila shaka msaada huo kwa familia ya Febe utapunguza machungu wanayopata yeye na wakimbizi wengine wa ndani kwenye eneo hilo kutokana na kuishi mbali na nyumbani na zaidi ya yote kulala nje.

Pamoja na kupatiwa misaada hiyo ya vifaa, hofu kubwa inayobakia miongoni mwa wakimbizi hao ni usalama hasa nyakati za usiku wakati ambapo visa vingi hutokea.