Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IFAD yakomboa wanawake Gambia

IFAD yakomboa wanawake Gambia

Kilimo bora kinahitaji pia uwepo wa ardhi yenye rutuba. Nchi Gambia kama ilivyo katika nchi nyingi za Afrika tunaelezwa kuwa ardhi yenye rutuba hutumiwa zaidi na wanaume na wanawake hubakia pembezoni kwenye ardhi iliyochoka na hivyo hata kwa jitihada gani matunda ya kazi ni nadra kuonekana. Lakini kwa sasa mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD umeleta matumaini kwa wanawake hao. Je nini kimefanyika? Ungana na Assumpta Massoi katika ripoti hii.

Ni wakati ambao msimu wa mvua umefikia ukingoni nchini Gambia, muda ambao akiba ya chakula kwa kawaida inakuwa ni kidogo. Wakati wanaume wanalima kwenye ardhi yenye rutuba, wanawake wao wanawalima mpunga kwenye ardhi iliyomomonyoka, isiyo na rutuba. Miongoni mwa wakulima hao wanawake ni Awa Jagne, mkulima wa mpunga.

(SAUIT YA AWA JAGNE)

"Hapa hakuna kitu ambacho kilikuwa kinastawi. Maji yalikusanyika kwa muda mfupi. Hata magugu yenyewe hayakuweza kustawi hapa.”

Awa Jagne ni mke wa nne na ndiye anayetegemewa zaidi na familia yake ya watoto Sita. Anasema kuwa mara nyinngi wanawake ndio wanakuwa na wajibu wa kulisha familia.

(SAUIT YA AWA JAGNE)

"Tuna wajibu wa kukidhi mahitaji ya msingi ya kaya zetu kama chakula, ada za shule na hata mavazi. Na ndio maana kila wakati wanawake wanakuwa hawana pesa inakuwa ni tatizo.”

Hata hivyo kwa msimu huu, hana wasiwasi wowote. Tofauti na wanawake wengine wengi nchini humo, Awa anaendelea kupatia chakula familia yake kwa kutumia mavuno ya msimu uliopita wa kilimo na hata ana ziada. Hii ni kutokana na teknlojia rahisi ambapo makinga maji pamoja na mifumo ya kutoa maji imejengwa katika mashamba yao na kufanya ardhi kuwa na rutuba zaidi. Hii ina maana kwa sasa wanaweza kuhifadhi maji ambayo awali yalikuwa yanapotea na kusababisha hata mmomonyoko wa ardhi yenye rutuba. Mifumo hiyo ilijengwa kutokana na mradi wa serikali unaofadhiliwa na IFAD. Chini ya mradi huo wameweza kurejesha ardhi inayotumika kwa kilimo. Jirani na eneo lao, eneo lililokuwa limegeuka oevu sasa linabadilishwa kuwa ardhi ya kilimo. Hadi sasa zaidi ya hekta Elfu 34 zimesharejeshwa kwa ajili ya kilimo.Mradi huo wa kutokomeza umaskini unalenga kuongeza uzalishaji wa chakula na vipato vya wananchi. Na kwa mujibu wa afisa wa IFAD, Moses Abubakari, ili kufanikisha hilo, ni lazima wanawake wawe na fursa ya kulima kwenye ardhi yenye rutuba.

(SAUTI YA MOSES ABUBAKAR)

"Ardhi yenye rutuba inatumiwa na wanaume. Wanawake hawana eneo la kulima. Kwa hiyo tumebaini kuwa kwa kutumia teknolojia rahisi tunaweza kusaidia nchi kupata ardhi zaidi na wanawake wanaweza kulima mpunga kwa sababu mchele ni chakula kikuu cha nchi hii.”

Hata hivyo haitoshi kwa wanawake kuwa na uwezo wa kutumia ardhi yenye rutuba pekee, bali pia wanahitaji fedha ili kuendeleza na kupana uzalishaji wao. Lakini benki za biashara zinasita kuwekeza vijijini.

(SAUTI YA MOSES ABUBAKAR)

"Benki ya kibiashara, moja ya sababu kuwa hawawezi kuwekeza vijijini ni kwabma kilimo ni cha msimu na kinaweza kupatwa na majanga makubwa.”

Kwa mantiki hiyo basi, IFAD inasaidia vyama vya kuweka na kukopa vya vijijini, SACCOS ambavyo huendeshwa na wakulima wenyewe. Mama B. Ceesay ni mwanachaam wa nne kujiunga na chama cha kuweka na kukopa kwenye eneo lake ambacho kina wanachama zaidi ya Elfu Mbili. Baada ya kuweka akiba ya kutosha sasa anaweza kuchukua mkopo.

Kwa kutumia mikopo, Mama ameongeza maradufu eneo lake la kilimo na amenunua punda na mkokoteni kwa ajili ya kusafirisha mavuno yake. Sasa ana chakula kingi kuliko hata mahitaji yake.

(SAUTI YA MAMA B. CEESAY)

"Kwa sasa wakati wowote familia yangu ikihitaji nina chakula cha kuwapatia. Hata wale wasio familia yangu. Nina furahia kumsaidia yeyote anayekuja nyummbani kwangu.”

Zaidiya watu Elfu 80, akiwemo Mama na Awa wananufaika na mradi wa kilimo unaotumia ardhi ambayo awali ilikuwa imeporomoka. Na kadri wanawake wengi wanavyopata ardhi yenye rutuba na pesa, ndivyo familia nyingi zaidi zitakuwa na chakula kwa kipindi chote cha mwaka.

Naam asante sana Assunpta Massoi kwa ripoti hiyo nami ni Monica Morara asante na kwaheri kwa sasa.