Takwimu mpya zadokeza idadi ya vifo nchini Syria kuwa zaidi ya Elfu 60

2 Januari 2013

Kamishna Mkuu wa Tume ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Navi Pillay amesema takwimu mpya zinadokeza idadi ya watu waliokufa nchini Syria kutokana na mapigano yanayoendelea ni zaidi ya Elfu 60.

Amesema upembuzi wa awali wa takwimu uliofanywa na wataalamu wa taarifa kwa niaba ya Umoja wa Mataifa umewezesha kukusanywa orodha ya watu Elfu Hamsini na Tisa Mia Sita Arobaini na Wanane walioripotiwa kuuawa kati ya tarehe 15 Machi hadi 30 Novemba mwaka jana.

Bi. Pillay amesema kwa kuzingatia kuwa mzozo huo umekuwa ukiendelea tangu mwisho wa mwezi Novemba inawezekana kukadiria kuwa watu Elfy 60 wameuawa hadi mwanzoni mwa mwaka 2013 na kwamba idadi hiyo ni kubwa kuliko walivyotarajia na inatisha.

Amesema hawajaweza kuthibitisha mazingira na sababu za kila kifo kwa sababu ya mazingira ya mzozo wenyewe na pia kwa kuwa hawajaruhusiwa kuingia Syria tangu mzozo uanza mwezi Machi mwaka 2011.

Upembuzi huo wa takwimu ulifanyika kwa miezi mitano na ulihusisha orodha ya visa zaidi ya Laki Moja na Elfu Arobaini ya vifo vya watu waliotambuliwa kwa majina yao pamoja na tarehe na eneo la tukio.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter