Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dhuluma ya kingono imekithiri Jamhuri ya Afrika ya Kati: Bangura

Dhuluma ya kingono imekithiri Jamhuri ya Afrika ya Kati: Bangura

Wanawake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao wamezingirwa na mzozo na kujikuta wakikumbwa na vitendo vya dhuluma ikiwemo kubakwa wamesema wamechoshwa na hali hiyo na sasa wanataka amani na wenzao wanaoshikiliwa na waasi waachiwe huru.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya ukatili wa ngono kwenye mizozo, Zainab Hawa Bangura amesema huo ndio ujumbe aliopewa na wanawake hao alipokutana nao wakati wa ziara yake nchini humo hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani, Bi. Bangura ameita mzozo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwa ni mzozo uliosahaulika na kwamba waasi wanabaka wanawake, wanatumikisha wasichana na kuandikisha wavulana kwenye jeshi kiasi kwamba hakuna shughuli ya kiuchumi, kisiasa au kijamii inayoweza kufanyika na hata hali ya usalama ni tete.

(SAUTI BANGURA)

Hata hivyo Bi. Bangura amesema ametia saini taarifa ya pamoja na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na pia waasi, ambapo pande hizo zimeridhia kulinda wanawake na watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kingono