Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali nchini Syria bado ni mbaya, Baraza la Usalama lichukue hatua: Brahimi

Hali nchini Syria bado ni mbaya, Baraza la Usalama lichukue hatua: Brahimi

“Hali ya usalama nchini Syria bado ni mbaya” ni kauli ya mjumbe maalum wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za kiarabu nchini Syria, Lakhdar Brahimi aliyoitoa mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama la umoja huo mjini New York, Marekani.

Bwana Brahimi amewaambia waandishi wa habari kuwa ametoa ujumbe huo alipohutubia baraza hilo juu ya hali ya usalama nchini Syria, ujumbe ambao pia amesema ndio atakaolipatia baraza kuu la Umoja wa Mataifa atakapolihutubia kesho Ijumaa.

“Hali chini Syria ni mbaya na inazidi kuzorota, bahati mbaya pande husika haziko tayari kuwa na suluhisho lao wenyewe, ukanda wa eneo hilo nao kwa sasa hauna uwezo kusaidia suluhisho la amani. Mahali ambako suluhisho la amani linaweza kuanzishwa ni baraza la usalama. Nimetakiwa kuandaa mpango, nafikiri kwa sasa tuna mwelekeo wa mpango huo lakini hatuwezi kuweka pamoja mpango huo hadi baraza hili litakapokubaliana kupitisha azimio litakalokuwa msingi wa mchakato wa amani wa kisiasa.”

Bwana Brahimi amesisitiza kuwa hatma ya Syria hata hivyo iko mikononi mwa wasyria wenyewe ambao ndio wataamua aina ya serikali wanayoitaka na si vinginevyo.