Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa kidini na kisiasa watumie ushawishi wao kwa maslahi ya umma: Ban

Viongozi wa kidini na kisiasa watumie ushawishi wao kwa maslahi ya umma: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema ni muhimu viongozi wa dini na wale wa kisiasa wakatumia ushawishi wao kwa maslahi ya umma huku akigusia matukio ya hivi karibuni huko Mashariki ya Kati na Mali yaliyoonyesha faida ya kuendeleza mahusiano mazuri na ya muda mrefu.

Amesema mjini Vienna, Austria wakati wa uzinduzi wa kituo cha kimataifa cha Mfalme Abdullah Bin Abdulaziz cha mashauriano ya utangamano wa kidini na kitamaduni na kuongeza kuwa matukio hayo yanadhihirisha umuhimu wa kuendeleza uhusiano mzuri na wa muda mrefu bila kujali tofauti za dini, utaifa, utamaduni, kabila na uraia.

Bwana Bwana amesema kwa kuzingatia hilo ndio maana ana imani kubwa na dira ya kituo hicho ya kuendeleza heshima ya utu wa mtu, haki za binadamu na kuchochea ushirikiano katika kuleta haki, maelewano na amani.

Ametaka kituo hicho kufanya kazi kwa karibu na ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu uimarishaji wa utengamano baina ya watu wa tamaduni tofauti, ambayo imepanga kukutana mwezi Februari mwakani

Akiwa Vienna, Bwana Ban pia alikuwa na mazungumzo na Rais wa Austria Heinz Fischer na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo ambapo wamejadili masuala kadhaa ikiwemo mchakato wa amani Mashariki ya Kati, hali huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Mali, Misri na Syria pamoja na Ulaya Mashariki.

Bwana Ban anatarajiwa kurejea New York, kesho mchana.