Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lalaani vikali mashambulizi ya waasi wa M23 mashariki mwa DRC

Baraza la usalama lalaani vikali mashambulizi ya waasi wa M23 mashariki mwa DRC

Wanachama wa Baraza la Usalama, wamelaani vikali mashambulizi ya waasi wa M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwenye maeneo ya Kibumba, Mboga na Ruhondo, pamoja na kuendelea kuukaribia mji wa Goma. Katika azimio lililofikiwa baada ya kikao maalum mjini New York siku ya Jumamosi, wanachama hao wa Baraza la Usalama pia wamewataka waasi hao kuheshimu majukumu ya vikosi vya usalama vya Umoja wa Mataifa, MONUSCO, na kuonya dhidi ya kujaribu kudhalilisha juhudi za MONUSCO.  Rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu, Balaozi Hardeep Singh Puri alisoma taarifa ya azimio hilo.

Baraza hilo pia limeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa idadi ya watu wanaolazimika kuhama makwao na wakimbizi, na kuwataka wahusika, hasa waasi wa M23, wajizuie na kuruhusu wahudumu wa kibinadamu kuwafikia wanaohitaji misaada kwa usalama, haraka na bila vizuizi. Pia limetoa wito kwa wote wanaotoa msaada kwa waasi wa M23 wakome kufanya hivyo. Katika azimio hilo, wanachama wa Baraza la Usalama pia wametoa wito kwa mataifa yaliyo na ushawishi kwa waasi wa M23 yawashawishi waasi hao wakomeshe mashambulizi.

Mkutano huo wa Baraza la Usalama uliitishwa kufuatia ombi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kutokana na hali ya usalama inayoendelea kuzorota. Baraza la Usalama limesema kamati namba 1533 itaundwa, ambayo itapokea mapendekezo ya mataifa wanachama, na baadaye hatua zitachukuliwa kulingana na mapendekezo hayo.

Wamerejelea umuhimu wa juhudi za Mkutano wa kanda ya Maziwa Makuu, ICGLR za kutafuta suluhu ya kisiasa, na kutoa wito kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuendelea na juhudi za ofisi zake za kuendeleza mazungumzo ya amani baina ya wahusika, na kuripoti kwa Baraza hili kuhusu mzozo huo katika siku chache zijazo.