Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili hali na maendeleo nchini Haiti

Baraza la Usalama lajadili hali na maendeleo nchini Haiti

Taifa la Haiti limekumbana na changamoto nyingi katika kipindi cha mwaka mmoja ulopita katika ngazi ya kisiasa na kibinadamu, na linahitaji kusaidiwa kujikwamua tena na kupiga hatua za maendeleo. Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu nchini Haiti, Nigel Fisher.

Bwana Fisher amesema hayo wakati akiwasilisha ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, MINUSTAH kwa Baraza la Usalama, ambalo limekutana kujadili hali nchini Haiti hii leo.

Bwana Fisher amesema ukuaji wa kiuchumi nchini Haiti ulishuka, huku ukosefu wa ajira ukiongezeka, na tufani na ukame kuathiri uzalishaji wa kilimo, kuathiri usalama wa chakula.

(SAUTI YA FISHER)

Ugonjwa wa kipindupindu unaendelea. Viwango vya vifo na maambukizi vimepunguka, ingawa kuongezeka tena mikurupuko hivi karibuni kunatia wasiwasi. Serikali imezindua mkakati wa kitaifa wa kuutomokomeza, ikisaidiwa na mpango wa Katibu Mkuu, ingawa ufadhili zaidi unahitajika. Hali ya usalama kwa ujumla imeimarika. Hata hivyo, hali ngumu ya kijamii na kiuchumi imeongeza maandamano ya umma.

Bwana Fisher amesema ripoti hiyo ya Katibu Mkuu ina mkakati wa malengo muhimu ya miaka mitatu ijayo yaloafikiwa na MINUSTAH na serikali ya Haiti, ili kuimarisha usalama, uongozi wa kisheria, udhibiti wa uchaguzi na kuendeleza taasisi za serikali.