Hakuna mfanyakazi wa kimataifa wa UNRWA aliyeondoka Gaza

15 Novemba 2012

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada na ulinzi kwa wakimbizi wa kipalestina, UNRWA limekanusha madai kuwa watumishi wake wa kimataifa wanaondoka Ukanda wa Gaza.

Msemaji wa UNRWA huko Gaza Adnan Abu Hasna amesema hayo huku akiongeza kuwa hali mbaya ya usalama imelazimu wasitishe shughuli zote za elimu ikiwemo kufunga shule hadi hali ya usalama itakapokuwa shwari.

UNRWA inakanusha kabisa taarifa za kuondoa wafanyakazi wake wa kimataifa. Badala yake wafanyakazi hao wataendelea na kazi na leo watumishi wane wameingia Gaza kusaidia operesheni za misaada tunazotekeleza katiak mazingira ya hatari.”

Katika hatua nyingine UNRWA imesema mwalimu wake mmoja ameuawa leo kwa kombora huko Kaskazini mwa Gaza wakati akiwa kwenye gari lake pamoja na kaka yake ambaye amejeruhiwa.

Kufuatia tukio hilo UNRWA imeelezea wasiwasi wake juu ya usalama wa raia huko Gaza huku ikiunga mkono wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon wa kutaka pande zote kwenye mgogoro huko Gaza kuepuka ghasia na waheshimu wajibu wao kwa mujibu wa sheria za kimataifa za haki za binadamu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud