Mtaalamu maalum wa UM kutembelea Sudan kutathmini hali ya kibinadamu

13 Novemba 2012

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa Chaloka Beyani kesho ataanza ziara ya siku Tisa nchini Sudan kuangalia hali halisi ya raia waliojikuta wakimbizi ndani ya nchi yao.

Ziara hiyo ya Beyani ambaye amepewa jukumu na baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kuchunguza madhila ya watu ambao ni wakimbizi ndani ya nchi zao inafuatia mwaliko wa serikali ya Sudan ambapo itampatia fursa ya kuzungumza na wakimbizi hao wa ndani na jamii zinazoathirika na uwepo wa wakimbizi hao.

Halikadhalika mtaalamu huyo atakuwa na mazungumzo na wawakilshi wa serikali na taasisi za kiraia, maafisa wa Umoja wa Mataifa na pande zingine ambapo watajadili uridhiaji wa mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu wakimbizi wa ndani pamoja na sera za kitaifa na sheria za kushughulikia kundi hilo.

Bwana Beyani amesema atakwenda pia Darfur kutathmini hali ya kibinadamu na hatimaye atatoa mapendekezo.

Ripoti kamili ya mtaalamu huyo itawasilsihwa kwenye baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Juni mwakani.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter