Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko yaanza kupungua taratibu Nigeria: OCHA

Mafuriko yaanza kupungua taratibu Nigeria: OCHA

Mafuriko yaliyokumba Nigeria kutokana na mvua zilizonyesha kati ya mwezi Julai na Oktoba mwaka huu yameanza kupungua wakati huu ambapo mamlaka ya hali ya hewa nchini huumo imetangaza kuwepo kwa mvua zaidi mwezi ujao zenye uwezekano mdogo wa kuleta madhara.

Ripoti ya awali ya hali halisi ya mafuriko nchini Nigeria iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA imesema kuwa idadi ya watu walioko kwenye makazi ya muda imepungua kwa kuwa wengi wao wanahifadhiwa kwa ndugu na jamaa na wengine wamerejea nyumbani.

Taarifa hiyo imesema kuwa kati ya watu zaidi ya Milioni Saba na Nusu walioathirika na mafuriko hayo, Milioni Mbili na Laki Nne wamejiorodhesha kama watu waliopoteza makazi yao na hivyo wanasubiri kupata misaada.

Kwa mujibu wa OCHA serikali ya Nigeria imetangaza kuwa itatoa dola Milioni Mia Moja na Kumi kwa ajili ya misaada huku wahisani wakitangaza mpango wa dola Milioni 38.

Mafuriko hayo mabaya zaidi kuwahi kukumba Nigeria ndani ya kipindi cha miongo minne yalisababisha vifo vya watu 363 huku zaidi ya 18,200 wakijeruhiwa na nyumba zaidi ya Laki Sita zikiharibiwa.