Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jitihada za kutokomeza Polio zinaendelea vizuri: WHO

Jitihada za kutokomeza Polio zinaendelea vizuri: WHO

Wakati leo ni siku ya kutokomeza Polio duniani, shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO limesema jitihada za kumaliza ugonjwa huo zinaendelea vizuri licha ya kwamba bado ugonjwa huo ni tishio nchini Nigeria, Afghanistan na Pakistani.

WHO imesema kuwa nchi hizo zimekuwa na jumla ya wagonjwa 166 wa Polio kati ya watoto 171 waliougua ugonjwa huo mwaka jana pekee duniani kote huku ikisema kuwa India imeondolewa kwenye orodha ya nchi zenye maambukizi ya Polio, wakati ni nchi ambayo ilidhaniwa kuwa ni vigumu zaidi kuutokomeza.

Msemaji wa WHO kwenye mradi huo wa kimataifa wa kupambana na Polio Oliver Rosenbauer amesema shirika hilo linasaidia utekelezaji wa mipango ya dharura ya kitaifa katika nchi hizo tatu yenye lengo la kuongeza idadi ya watoto wanaopatiwa chanjo ya ugonjwa huo, mkakati ambao amesema ni muhimu katika kutokomeza Polio.

Inawezekana kutokomeza Polio, hakuna sababu kwa nini tushindwe. Tuna vifaa vyote muhimu vya kuutokomeza. Kwa hiyo sasa kilichobaki ni utashi wa kisiasa na wa kijamii kuhakikisha mipango ya dharura inapatiwa fedha na inatekelezwa. Tumeshuhudia mara kwa mara kuwa kirusi cha ugonjwa huu kinasambaa eneo ambako watoto hawajapatiwa chanjo na kusababisha mlipuko. Iwapo hatutamaliza kazi hii sasa, tutashuhudia katika muongo ujao wagonjwa wapya Laki Mbili duniani kote kila mwaka. Kwa kuwa sasa wagonjwa na chini ya Laki Moja kila mwaka tunaona kuwa ni janga la kibinadamu ambalo linapaswa kuepukwa kwa gharama zozote.”