Umoja wa Mataifa wasisitiza mshikamano wake na Lebanon

22 Oktoba 2012

Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya Lebanon Derek Plumbly na mabalozi wa nchi tano zenye ujumbe wa kudumu katika Baraza la Usalama la umoja huo wamekutana na Rais wa Lebanon Michel Sleiman mjini Baada na kuelezea mshikamano wao na nchi hiyo wakati huu wa kipindi kigumu.

Taarifa iliyotolewa imesema wakati wa mazungumzo na Rais Sleiman walirejelea taarifa iliyotolewa na Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa niaba ya wajumbe wa baraza hilo siku ya Ijumaa ya kushutumu shambulio lililosababisha kifo cha mkuu wa usalama Brigedia Jenerali Wissam Al Hassan na watu wengine na mamia kadhaa kujeruhiwa.

Wajumbe wa baraza hilo wametaka wahusika wa shambulio hilo la kigaidi wafikishwe mbele ya sheria na kuelezea utayari wao wa kuunga mkono hatua zozote za serikali ya Lebanon za kuondokana na vitendo vya kukwepa mkono wa sheria.

Halikadhalika wamekumbusha wito kwa pande zote zinazopingana nchini Lebanon kuendeleza umoja wa kitaifa pindi majaribio ya kuleta vurugu yanapoibuka huku wakipongeza uongozi wa Rais Sleiman wakati huu wa mashauriano yake na vyama vyote nchini humo ya kuleta amani, utulivu na usalama.

Wakati huo huo ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Lebanon imefuta sherehe za siku ya Umoja huo zilizokuwa zifanyike keshokutwa mjini Beirut, ikiwa ni hatua ya kuungana na wananchi wa Lebanon kuomboleza vifo vilivyotokana na shambulio la Ijumaa huko Ashrafieh.

Badala yake fedha zilizokuwa zitumike kwenye shughuli hiyo zitapatiwa wakazi wa eneo liliathiriwa na shambulio hilo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud