Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wa Syria unaweza kuenea zaidi:Ban

Mgogoro wa Syria unaweza kuenea zaidi:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameonya kuwa mgogoro wa Syria unazidi kuongezeka na unaweza kuwa tishio kwa nchi jirani za ghuba na hata eneo lote.

Akifungua mkutano wa jukwaa la kimataifa la demokrasia lilioandaliwa na Baraza la Ulaya huko Strasbourg Ufaransa, Ban amesema ongezeko la uhasama katika mpaka wa Syria na Uturuki na athari za mgogoro huo nchini Lebanon zimetikisa utulivu wa eneo hilo.

Ameitaka serikali na vikundi vya upinzani nchini Syria kukataa vurugu na badala yake kushiriki katika majadiliano kwa maslahi ya raia wa nchi hiyo na kwamba mpango wa kupatia silaha serikali na majeshi ya upinzani ukome.

Kitendo cha kuwapatia silaha kinfanya hali kuwa mbaya zaidi na kuwatia wananchi wa Syria matatani. Natoa wito kwa pande zote husika kuacha na vurugu na kutafuta suluhisho la kisiasa. Hiyo ndio njia pekee ya kumaliza mgogoro huu. Syria inaonyesha jinsi kipindi cha sasa cha mpito kilivyoleta matumaini na mabadiliko lakini pia kimeibua wasiwasi na hofu. Bado ninashawishika kuwa tunalazimika kutafuta suluhisho la kisiasa katika mgogoro huu wa Syria .”