Dhuluma kwa wanawake na wasichana ni kati ya changamoto zinazokumba jamii za kiasili
Dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana na kuporwa kwa mali asili ni kati ya changamoto zinazozikumba jamii za asili kwa sasa amesema mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wa asili James Anaya. Mwaka uliopita Anaya alifanya ushirikiano na mataifa kadha, mashirika ya Umoja wa Mataifa na jamii za kiasili kwenye utafiti wa kuelewa changamoto zinazowakumba watu wa asili kila siku.
Anaya amesema kuwa kwenye mazungumzo na waakilishi wa masuala ya watu wa asili walisisitiza umuhimu kwa kufanya jitihada za kumaliza dhuluma dhidhi ya wanawake na wasichana kutoka jamii za kiasili. Akihutubia baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva Anaya amesema kuwa kati ya haki wanazostahili kuhakikishiwa watu wa jamii za kiasili ni pamoja na haki ya kumiliki mali, ardhi na mali asili, haki za kuendeleza utamaduni, haki ya dini na afya.