Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ahimiza ushirikiano katika kutumia upatanishi kutatua mizozo

Ban ahimiza ushirikiano katika kutumia upatanishi kutatua mizozo

Umoja wa Mataifa na wadau wengine wanapaswa kushirikiana na kutumia vyema uwezo wa upatanishi katika kuzuia, kudhibiti na kutatua mizozo na migogoro. Huo umekuwa ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon kwa Baraza Kuu siku ya Alhamis, wakati akizindua ripoti yake kuhusu suala hilo.

Bwana Ban amesisitiza kuwa upatanishi si wajibu wa Umoja wa Mataifa pekee, kwani mataifa wanachama, mashirika ya kikanda, na mashirika yasiyo ya kiserikali yanahusika zaidi mara kwa mara.  Amesema uwepo huu wa wahusika wengi ni kitu cha kuaziziwa, kwani kila mmoja anaweza kuchangia katika kutafuta amani, kulingana na uwezo alio nao. Hata hivyo, amesema kuwa ushindani miongoni mwa wahusika umelegeza juhudi za kupatanisha.

Amesema ni wajibu wa ulimwengu wote kwa pamoja kushirikiana na kuunga mkono matumizi bora ya upatanishi. Katibu Mkuu amesema Umoja wa Mataifa unashirikiana na wadau wengine ili kuongeza uwezo wa huduma za upatanishi, na kushirikiana na mitandao yote kwenye ngazi za kikanda, kitaifa na hata mikoani.