Wapalestina 250,000 walioko Syria wanahitaji msaada zaidi:UNRWA

12 Septemba 2012

Takriban wakimbizi 250, 000 wa Kipalestina ambao wanaishi Syria wanahitaji misaada ya kibinadamu, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowasaidia Wapalestina, UNRWA. Shirika la UNRWA limesema wakimbizi hawa wanahitaji zaidi vitu kama chakula, pesa na huduma za afya, na sasa limelazimika kufanyia marekebisho makadirio yake ya misaada wanayohitaji.

Idadi kubwa ya wakimbizi hao pia watahitaji kusaidiwa kwa njia ya kutumiwa pesa, kufuatia kufungwa kwa biashara zao ndogondogo ambazo zilikuwa zinasaidia kutoa nafasi za ajira kwao.

Shirika la UNRWA limetoa ombi la dola milioni 54 za kimarekani ili kuwasaidia Wapalestina hao, ambao wameathiriwa na mzozo wa Syria. Mkuu wa UNRWA, Filippo Grandi ametoa wito kwa nchi jirani ziwape hifadhi wakimbizi wa Kipalestina ambao huenda wakakimbia machafuko yanayoendelea Syria

Takriban wakimbizi 4,000 wa Kipalestina waliokuwa wanaishi Syria wamekimbilia Jordan na Lebanon.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter