Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wimbi la wakimbizi wa ndani Syria ni kutokana na kutoheshimu sheria za Kimataifa:UM

Wimbi la wakimbizi wa ndani Syria ni kutokana na kutoheshimu sheria za Kimataifa:UM

Kupuuza haki za binadamu za kimataifa na sheria za kimataifa kumechangia kuwepo kiasi kikubwa sana cha wakimbizi wa ndani nchini Syria, wakati mgogoro unapozidi kutokota, amesema mtaalam wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wakimbizi wa ndani, Chaloka Beyani.

Bwana Beyani ameelezea kusikitishwa kwake na hali ya takriban watu milioni 1.5, ambao wamelazimika kuhama makwao kufuatia ghasia nchini Syria na kuwa wakimbizi wa ndani nchini humo. Amesema mapigano makali na matumizi ya silaha nzito nzito katika makazi ya watu wengi ni jambo la kutia wasiwasi zaidi.

Ametoa wito kwa serikali ya Syria na pande zote katika mgogoro huo kuhakikisha sheria za kimataifa, zikiwemo sheria za haki za binadamu na sheria za kibinadamu zinaheshimiwa kwa hali yoyote ile, ili kuwalinda na kuwasaidia wakimbizi wa ndani, na kuzuia hali inayoweza kuchangia watu wengi zaidi kuwa wakimbizi wa ndani.