Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaweka Mchakato wa Kuwachukulia Hatua za Kisheria Wahalifu wa Ngono

UNHCR yaweka Mchakato wa Kuwachukulia Hatua za Kisheria Wahalifu wa Ngono

Visa vya ubakaji na dhuluma za ngono katika kambi ya wakimbizi ya Kiziba nchini Rwanda vinapungua, lakini athari za kimwili na hisia husalia kuwa kubwa visa hivi vinapotokea.

Desturi ya wakimbizi wa Kongo kwenye kambi hiyo kuvinyamazia visa hivi kila vinapotokea, inafanya mambo kuwa mabaya zaidi, kwani huendeleza kutowachukulia hatua za kisheria wale wanaovitenda, na kuwaacha waathirika kwenye hali ya ukiwa na uoga. Hii ndio maana Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi, UNHCR na wadau wengine, wanatoa kipaumbele kwa kupiga vita dhuluma za ngono katika kambi ya Kiziba na kuwatia moyo watu walizungumzie suala hilo.

Aghalabu waathirika, na hasa watoto, hawafahamu ni nini kimewafanyikia, na wale wanaoripoti visa hivi huonekana kubanwa na uoga wakisema walowatendea ukatili huo watawaua ikiwa watajua kwamba wameripotiwa.Shirika la UNHCR linatambua kuwa mojawepo wa shida kuu, ni kutowawajibisha wahalifu, na hivyo kuchagiza mtindo unaolenga kuwafikisha wahalifu kama hao mbele ya vyombo vya sheria. Mbali na haki, shirika hilo linaangazia uchungu wa kijamii na ule wanaopitia waathirika binafsi kufuatia dhuluma kama hizi, ili kuwasaidia na kuwapa matumaini mapya waathirika.