Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ahimiza Njia na Ari mpya Kuwalinda raia katika maeneo ya vita

Ban ahimiza Njia na Ari mpya Kuwalinda raia katika maeneo ya vita

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amelitaka Baraza la Usalama na mataifa wanachama kutafuta njia mpya za kuwalinda raia na kuhakikisha ukiukaji wa sheria za kimataifa na haki za binadamu unakabiliwa ipasavyo. Bwana Ban amesema haya katika ripoti yake ya tisa, wakati wa mjadala wa Baraza la Usalama kuhusu kuwalinda raia katika maeneo ya vita.

Akitoa mifano ya hivi karibuni ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na mauaji ya raia katika nchi za Afghanistan, Somalia, Sudan na Sudan Kusini, Syria, Ivory Coast na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Bwana Ban amesema, wahusika katika migogoro hawana budi kuheshimu sheria za kimataifa ili kuwalinda raia.

Amesema ni muhimu kuyafikia makundi yasiyo ya kitaifa katika migogoro na ujumbe wa kuyafanya yaelewe wajibu wao na athari za kukiuka sheria hizi, na kuwachukulia hatua za kisheria wanaozikiuka. Ameongeza kuwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa vinapopewa jukumu la kuwalinda raia, ni lazima vipewe vifaa vya kutenda kazi na ufadhili unaotosheleza kutimiza majukumu yao, na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia raia.