Kuna hatari ya kurejea ukatili wa kimapenzi Mashariki mwa Congo:Wahlstrom

3 Mei 2012

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kimapenzi kwenye maeneo ya vita Margot Wahlstrom amezitaka pande zote Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kusitisha mara moja vitendo vyovyote vya ghasia na ameitaka serikali ya nchi hiyo kurejesha udhibiti wake na kuhakikisha raia wanalindwa, katika eneo hilo kutokana na vitendo vya ukatili ukiwemo ubakaji.

Katika taarifa yake Bi Wahlstrom ameelezea hofu yake kuhusu kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama Mashariki mwa Congo kufuatia mapigano makali baina ya vikosi vya serikali na makundi ya wanamgambo waasi yenye silaha.

Amesema mashaka yake makubwa ni katika vijiji vya eneo la Walikale Kivu ya Kaskazini ambayo yameghubikwa na makundi ya waasi na yaliyokumbwa na uhalifu mkubwa mwei Julai na Agosti mwaka 2010 ambapo wanawake, wanaume na watoto 387 walibakwa na makundi hayo ya wapiganaji.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud