Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake bado wanalipwa robo tatu ya fedha wanazolipwa wanaume:UNCTAD

Wanawake bado wanalipwa robo tatu ya fedha wanazolipwa wanaume:UNCTAD

Sera za uchumi ni lazima ziangalie zaidi mahitaji ya wanawake na kuchagiza kufikia malengo ya maendeleo yanayojumuisha wote. Huu ni ujumbe uliotolewa na mkuu wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa biashara na maendeleo kwenye kongamano linalofanyika Doha Qatar.

Mkutano wa wanawake na maendeleo unakwenda sambamba na ule wa UNCTAD ambapo pia unafanyika Doha.

Lengo la mkutano huo ni kuchagiza sera ambazo zinawawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika masuala ya uchumi na jamii.

Mkuu wa UNCTAD Supachai Panitchpakdi amesema katika muongo uliopita tofauti za kipato na kutokuwepo usawa wa kijamii kumeongezeka. Amesema hii inaonekana dhahiri katika pengo lililopo baina ya wanaume na wanawake katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea.

Wanawake bado wanalipwa asilimia 75 ya mishahara wanayolipwa wanaume katika sekta zisizo za kilimo na wanawake ni asilimia 45 ya nguvu kazi ya dunia. Na wanawake wanashika asilimia 70 ya watu wote masikini duniani.

Amesema suala la kutokuwepo usawa sio tu linatoa changamoto kwa watunga sera lakini pia linaweza kuwa chanzo cha kutokuwepo hali ya utulivu wa kiuchumi na kijamii na pia kurudisha nyuma maendeleo.