Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yapeleka kwa ndege msaada wa chakula Chad

WFP yapeleka kwa ndege msaada wa chakula Chad

Shirika la Umoja wa mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limekamilisha kupeleka kwa ndege msaada wa haraka wa lishe kwa maelfu ya watoto walio katika hatari ya kupata utapiamlo nchini Chad, taifa ambalo limekumbwa na ukame.

Ndege mbili zimewasili Ndjamena wiki hii na leo malori yataanza kubeba karibu tani 200 za msaada wa haraka wa chakula ukiwa ni pamoja na karanga zilizosagwa kuzuia utapia mlo katika maeneo yaliyoathirika zaidi na ukame.

Watoto takribani 36,000 wa chini ya miaka miwili katika majimbo ya Wadi-Fira na Sila Mashariki mwa Chad watapokea msaada unaofadhiliwa na idara ya tume ya misaada ya kibinadamu barani Ulaya ECHO.

Utapia mlo uliokithiri unaathiri asilimia 16 ya watoto Chad na hivyo kupindukia kiwango kilichowekwa cha asilimia 15, katika nchi zilizoathirika zaidi miongoni mwa nchi 22.

Hata kabla ya matatizo kuanza Sahel mwaka  jana kiwango cha utapia mlo nchini humo kiliwa ni asilimia 10.

Kama zilivyo nchi nyingi za Sahel Chad inakabiliwa na ukame wa hali ya juu uliosababisha uzalishaji wa chakula kushuka kwa asilimia 43 na kuwaacha watu milioni 3.5 katika hali mbaya, kati ya hao milioni 1.2 wanahitaji msaada wa haraka.