Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uamuzi dhidi ya Lubanga ni hatua kubwa katika vita dhidi ya Ukatili:Pillay

Uamuzi dhidi ya Lubanga ni hatua kubwa katika vita dhidi ya Ukatili:Pillay

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay Jumatano amepongeza uamazi wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC dhidi ya kesi ya bwana Thomas Lubanga, ambaye amekutwa na hatia ya kuwaingiza na kuwatumia watoto jeshini huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kati ya mwaka 2002 na 2003.

Bi Pillay amesema hukumu hiyo ni hatua kubwa kwa haki ya kimataifa na ni hatua kubwa katika vita dhidi ya ukatili. Ameongeza kuwa kwa miaka mingi na kila siku dunia imekuwa ikiorodhesha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliotekelezwa na Lubanga dhidi ya watu wa Congo, na uamzi dhidi yake leo unatuma ujumbe mahususi katika kupinga ukatili na kiukwaji wa sheria za kimataifa.

Amesema wakati jukumu kubwa la kuwachukulia hatua wakiukaji wa haki za binadamu katika ngazi ya kitaifa, lakini ICC ina jukumu kubwa, wakati mataifa hayo yanaposhindwa au kutokuwa tayari kuhakikisha haki inatendeka kwa makosa makubwa ya kimataifa kama uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari.