Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zaridhia mpango wa kulinda mazingira ya bahari

Nchi zaridhia mpango wa kulinda mazingira ya bahari

Nchi 65 ambazo zinahudhuria mkutano wa kimataifa huko Philippine zimepiga hatua kwa kukubali kuunga mkono maazimo yenye shabaha ya kulinda mazingira ya bahari yanayoandamwa na athari kutokana na shughuli za kibinadamu zinazofanywa katika nchi kavu.

Nchi hizo zimesema kuwa kuna haja ya kuweka utashi wa pekee ili kuhakikisha maeneo hayo yanapewa kipaumbele na kuepushwa na athari zozote zinazoweza kuharibu sura kamili ya maeneo hayo.

Wajumbe kutoka nchi hizo 65 wanaohudhuria mkutano huo unaoratibiwa na Umoja wa Mataifa wameafiki kuanzishwa kwa shabaha hiyo mpya wakiamini kuwa ndiyo itayotoa mustakabala mwema kwa maeneo hayo.

Mkutano huo wa siku nne ulioandaliwa na serikali ya Philippine kwa kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na mazingira UNEP, umewajumuisha mawaziri,wataamu wa masuala ya mazingira pamoja na wasomi kadhaa.