UM wataka kuanzishwa kwa maridhiano DRC ili kuondoa mkwamo wa kisiasa

UM wataka kuanzishwa kwa maridhiano DRC ili kuondoa mkwamo wa kisiasa

Afisa wa Umoja wa Mataifa anayehusika na vikosi vya ulinzi wa amani, ambaye yuko ziarani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesisitiza udharura wa kuanzisha fursa ya maridhiano na utengamao wa kijamii ili kuondoa mkwamo na kuzorota kwa hali ya kisiasa inayoiandama nchi hiyo tangu kufanyika kwa uchaguzi wa rais Novemba mwaka jana.

Hervé Ladsous amesema kuwa wakati joto la kisiasa likiendelea kutoa picha ya wasiwasi na mashaka, kuna haja sasa kuwepo wa fursa ya maridhiano ili kuipusha nchi hiyo kutumbukia kwenye mzozo mkubwa zaidi.

Amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kutoa msukumo wa pekee kwa nchi za Afrika ili kuimarisha mifumo ya amani na utengamao wa kisiasa. Amekumbusha pia shabaha ya kuwepo kwa vikosi vya ulinzi wa amani MUNUSCO katika maeneo yenye mizozo akisema kuwa ni utashi wa Umoja wa Mataifa kuyafanya maeneo hayo yanajipushe na mizozo.