Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfuko mpya wa UM watoa dola 300,000 kusaidia waathirika wa usafirishaji haramu wa watu

Mfuko mpya wa UM watoa dola 300,000 kusaidia waathirika wa usafirishaji haramu wa watu

Mashirika kutoka nchi 12 yanayosaidia waathirika wa usafirishaji haramu wa watu ili waweze kupata haki, kurejea nyumbani na kurejea katika maisha ya kawaida kwa pamoja yamepewa dola 300,000 leo msaada kutoka mfuko mpya wa Umoja wa Mataifa.

Mtazamo huo umechukuliwa na Umoja wa Mataifa ili kutoa msaada wa fedha unaohitajika kwa waathirika wa uhalifu wa kusafirishwa kwa njia haramu amesema mkurugenzi mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uhalifu na madawa UNODC Yury Fedotov.

Ameyasema hayo alipokuwa akiomba msaada wa fedha kwa mfuko huo ulioanzishwa mapema mwaka huu kama sehemu ya UNODC inayodhibiti mfuko wa hiyari wa Umoja wa Mataifa kusaidia waathirika wa usafirishaji haramu wa watu. Amesema hakuna nafasi ya ukatili huo hapa duniani na mfuko huo mpya una jukumu la kuhakikisha vitendo hivyo visivyo vya kibinadamu vinatokomezwa.

Biashara haramu ya kusafirisha watu inakadiliwa kuwa ni ya dola bilioni 32 na kwa sasa takribani watu zaidi ya milioni 2.4 wamesafirishwa kiharamu huku theluthi mbili ni wanawake na watoto.

Miradi 12 iliyochaguliwa kupata msaada ni kutoka kanda zote za dunia na inagusa maeneo ya Albania, Cambodia, Costa Rica, Jamhuri ya Czech, Ufaransa, India, Israel, Kenya, Nepal, Nigeria, Moldova na Marekani.