Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO ijikite sasa katika kuleta maendeleo:Kabila

MONUSCO ijikite sasa katika kuleta maendeleo:Kabila

Wakati amani imeanza kurejea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo ametoa wito wa kubadili jukumu la mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo ambao umesaidia kuleta amani na utulivu katika eneo kubwa la nchi hiyo na kujikita katika maendeleo ya uchumi.

Rais Kabila amesema ni muhimu mtazamo wa MONUSCO yenye wanajeshi 19,000 nchini humo kusaidia katika maendeleo ya watu wa taifa hilo kubwa Afrika.

Tangu mwaka 1999 ukiwa na majina kadhaa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Congo umeshuhudia taifa hilo likiibuka kutoka kwenye miongo ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, machafuko mbalimbali na hatimaye 2006 uchaguzi wa kwanza wa kidemkrasia baada ya takribani miongo minne, ingawa bado hadi sasa mapigano bado yanaendelea katika eneo la Mashariki mwa nchi ambako vikosi vya Umoja wa Mataifa vimepelekwa.

Uchaguzi mkuu umepangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu na Rais Kabila na serikali yake amesema wanachukua hatua zote muhimu kuhakikisha unakuwa huru, wazi na wa haki na kufanyika kwa amani.

Kabila amesema taifa lake bado linakabiliwa na changamoto nyingi na linahitaji msaada wa MONUSCO ikiwemo kufanyia mabadiliko jeshi, polisi na mfumo wa sheria, pia kurejea nyumbani kwa wakimbizi wa ndani na nje, na suala la kuwarejesha katika maisha ya kawaida watoto wanaotumika vitani na makundi ya wanamgambo mbalimbali.

Mwezi Juni mwaka huu baraza la usalama liliongeza kwa mwaka mmoja zaidi muda wa MONUSCO baada ya mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Congo Roger Meece kusema kumekuwa na hata kubwa za kimarika kwa usalama licha ya changamoto ambazo bado zinaendelea.