Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO kuzindua mpango wa elimu kwa wasichana

UNESCO kuzindua mpango wa elimu kwa wasichana

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya elimu, sayansi na utamaduni UNESCO linatazamiwa kuzindua mpango maalumu utaowasaidia wanawake na wasichana kupata elimu.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Bi Irina Bokova anatazamiwa kuwakaribisha wageni kwenye uzinduzi huo unaotazamiwa kufanyika May 26, kwenye makao makuu ya shirika hilo mjini Paris.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bi Hillary Clinton wanatazamiwa kutoa hotuba kwenye uzinduzi huo.

Mpango huo unataka kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja kwenye kiwango cha kimataifa ili kuhakikisha kwamba mamia kwa maelfu ya watoto wa kike na kina mama wanapatiwa elimu.

Zaidi ya wasichana milioni 39 duniani kote ambao wanastahili kuwa kwenye elimu ya sekondari wameendelea kukosa nafasi hiyo wakati kundi kubwa la watu wasiojua kusoma na kuandika ni wanawake.