Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban amesema UM utaendelea kuisaidia DR Congo ikielekea uchaguzi mkuu mwaka huu

Ban amesema UM utaendelea kuisaidia DR Congo ikielekea uchaguzi mkuu mwaka huu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema operesheni za Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni moja ya operesheni kubwa kabisa na yenye changamoto nyingi. Akizungumza kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ambalo leo linajadili hali ya Congo Ban amesema kuna masuala makubwa manne ambayo kwanza ni usalama na kuwalinda raia hali ambayo kiasi imeimarika kutokana na juhudi za serikali na mpango wa Umoja wa Mataifa MONUSCO, upokonyaji silaha na kuwarejesha katika maisha ya kawaida askari waasi.

Lakini amesema makundi ya wapiganaji wa kigeni na ya congo yanaendelea kutoa tishio, ukiukaji wa haki za binadamu, mauaji, ubakaji,uporaji na kuchomwa kwa vijiji, kulikosababisha mamilioni ya watu kuwa wakimbizi wa ndani na nje.

Pili amesema uchaguzi ujao wa mwezi Novemba lazima ufanyike kwa wakati, kwa uwazi na bila bughdha.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Ban pia amezungumzia utawala wa sheria, uongozi na ujenzi wa taasisi akisema amani ya kudumu ya nchi hiyo inahitaji nguzo hizo ambazo zitatoa huduma muhimu, usalama na kufuata sheria kwa wote. Na mwisho amesema maendeleo ya kiuchumi ni muhimu sana na Congo haiwezi kuwa na utulivu wa kudumu bila ujenzi mpya na maendeleo.