Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanamgambo wanaendeleza mashambulizi Ivory Coast

Wanamgambo wanaendeleza mashambulizi Ivory Coast

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA limesema makundi ya wanamgambo wenye silaha yameendelea kufanya mashambuli dhidi ya raia Magharibi mwa Ivory Coast.

Kwa mujibu wa ripoti ya pamoja iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, shirika la kimataifa la uhamiaji na OCHA machafuko yamekuwa kikwazo kikubwa kwa wafanyakazi wa misaada kuwafikia maelfu ya watu walioamua kutokimbia na kwa sasa wanahitaji msaada wa maji, madawa na chakula.

Mashirika hayo yanasema mrundikano wa watu katika kanisa Katoliki mjini Duekoue ambako watu 28,000 hivi sasa wanahifadhiwa ni suala linalowatia hofu na wamesema kuna haja ya haraka ya kufungua kituo kingine ili kuboresha hali ya wakimbizi wa ndani nchini humo.

Nalo shirika la afya duniani WHO limesema limehitimisha limehitimisha zoezi la usaili Magharibi mwa Ivory Coast. WHO inasema katika mikoa ya Montagnes na Moyen asilimia 52 ya vituo vya afya na asilimia 62 ya hospitali hazifanyi kazi kutokana na upungufu wa wahudumu wa afya, kuporwa kwa madawa na bvifaa vya tiba, kuharibiwa kwa miundombinu na usalama mdogo.