Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Libya kukabiliwa na matatizo makubwa ya chakula kama hatua hazitochukuliwa kusaidia:WFP

Libya kukabiliwa na matatizo makubwa ya chakula kama hatua hazitochukuliwa kusaidia:WFP

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP limesema linatiwa hofu na hali ya usalama wa chakula nchini Libya ambako kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa machafuko yamekuwa yakiendelea kwenye miji mbalimbali ikiwemo Tripoli, Misrata na Benghazi.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva hii leo kuhusu hali ya usalama wa chakula nchini Libya mkuu wa WFP kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini Daly Belgasan amesema nchi hiyo imebakia na akiba ndogo ya chakula cha kutosheleza muda usiozidi miezi miwili na endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa kuongeza akiba ya chakula basi kutakuwa na matatizo makubwa.

(SAUTI YA DALY BELGASAN)

WFP pia imesema inahofia upatikanaji wa chakula kwa maelfu ya watu waliokwama kwenye maeneo yenye mapigano makali, wakimbizi wa ndani, wahamiaji na makundi ya watu wasiojiweza.

Shirika hilo limesema jinsi vita vinavyoendelea kwa muda mrefu idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula pia inaongezeka. Libya ni muagizaji mkubwa wa chakula kutoka nje na machafuko yamefanya kuwa vigumu kuingiza chakula cha kutosha.