Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mikakati ya kudhibiti mihadarati ifikiriwe upya:UNODC

Mikakati ya kudhibiti mihadarati ifikiriwe upya:UNODC

Afisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa nchi kufikiria upya mikakati ya kimataifa ya udhibiti wa madawa huku kukiwa na changamoto ya madawa hayo kuwa tishio kwa afya ya jamii, usalama na maendeleo.

Afisa huyo ambaye ni mkurugenzi wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya madawa na uhalifu UNODC bwana Yury Fedotov amesema nchi wanachama na mashirika ya Umoja wa Mataifa lazima kutambua kwamba madawa pamoja na uhalifu wa kupangwa ni tishio la kufikia malengo ya maendeleo ya milenia hapo 2015.

Amesema udhibiti wa mihadarati ni lazima uwe kipengee muhimu katika juhudi za pamoja za kufikia malengo ya afya, usalama na maendeleo. Bwana Fedotov ameyasema hayo katika ufunguzi wa kikao cha 54 cha tume inayohusika na mihadarati ambayo ni bodi ya sera ya masuala yanayohusiana na madaya ya Umoja wa Mataifa inayokutana mjini Vienna hadi Ijumaa.

Amesema kwa baadhi ya nchi na mabara thamani ya fedha zitokanazo na mihadarati zinazidi hali ya uchumi halali wa nchi hizo, na kwa sasa wasafirishaji wa madara haramu na uhalifu wa kupangwa umeunda mtandao wa kimataifa na matokeo yake kuna ongezeko la ghasia, vita na ugaidi unaochagizwa na usafirishaji haramu wa mihadarati na uhalifu wa kupangwa.