Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mastaa wa Hollywood wasaidia kuzindua mfuko kusaidia waliosafirishwa kiharamu

Mastaa wa Hollywood wasaidia kuzindua mfuko kusaidia waliosafirishwa kiharamu

Wanawake wengi wanaingizwa katika biashara ya ngono, wanaume wanalazimishwa kufanya kazi za vibarua katika kilimo, huku watoto wakishinikizwa katika kazi za ndani au biashara ya ngono.

Waathirika wa usafirishaji haramu wa watu wana sura nyingi, lakini kitu kimoja kilicho sawia kwa wote ni ukweli kwamba wameondolewa nchi kwao na kupelekwa nchi nyingine bila ridhaa yao na kwa faida ya magenge ya wahalifu waliowasafirisha kiharamu.

Wacheza filamu maarufu wa Hollywood Demi Moore na mumewe Ashton Kutcher wamesaidia kuzinduliwa kwa mfuko maalumu wa Umoja wa Mataifa kusaidia waathirika wa usafirishaji haramu wa watu. Uzinduzi huo umefanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa hapa New york.

Demi Moore amesema ametiwa hamasa ya kuchukua hatua baada ya kuangalia kipindi cha televisheni kuhusu wasichana wa Cambodia ambao wametekwa na kuuzwa kuwa watumwa wa ngono. Ameongeza kuwa ni kitu kisichokubalika na tukaona hatuwezi kukaa tuu na kuishi katika dunia hii bila kuchukua hatua yoyote dhidi ya hali hiyo. Kwa watoto hao ambao hawana hati ni kuwaingiza katika utumwa wa ngono ni kuwapora utoto wao.

Naye mumewe Ashton Kutcher ni mtaalamu wa masuala ya kuwasiliana katika mtandao, zaidi ya watu milioni sita wanamfuatilia kupitia twitter. Amesema kama nitatumia mtandao kufikisha ujumbe kwa wanaume wote duniani kwamba kununua ngono , kununua wasichana sio kitu kizuri, labda tunaweza kutumi ushawishi wetu kubadili tabia na kuelimisha kuhusu uhalifu huu. Labda tutawashawishi wanaume kupiga vita suala hili na tutabadili tabia zao.

Mastaa hao wamesaidia kuzindua mfuko wa hiyari wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya waathirika wa usafirishaji haramu wa watu ambao utawzishirikisha serikali, sekta binafsi, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na wadau wengine kusaidia kukomesha suala hili. Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya madawa na uhalifu

Yury Fedetov amesema usafirishaji haramu ni uhalifu wa kupangwa unaohusisha mabilioni ya dola.

Ni mtandao na wahalifu wako katika nchi A wakichukuwa wanyonge wao nchi B na kuwapeleka nchi C,wakisubiri kufikishwa malaha D. Hakuna nchi moja tuu inayoweza kukabili changamoto hii peke yake, ushirikiano wa kimataifa unahitajika.