Wahamiaji zaidi wawasili Lampedusa Italia:IOM

Wahamiaji zaidi wawasili Lampedusa Italia:IOM

Kuwasili kwa wahamiaji zaidi ya 1630 kwenye kisiwa cha Lampedusa Italia jana Jumapili na usiku wa kuamkia leo kumesababisha mrundikano mkubwa kwenye kituo cha wahamiaji ambapo IOM na washirika wake wanatoa msaada wa mapokesi na ushauri wa kisheria kwa wahamiaji, waomba hifadhi na watoto wasioambatana na mtu yeyote.

Kwa mujibu wa IOM idadi ya wahamiaji katika kituo imefikia 4780 wakati kituo hicho kina uwezo wa kupokea watu 800 tuu jambo lililosababisha mrundikano mkubwa.

IOM inasema wengi hawana huduma za usafi kama vyoo, na wamekuwa wakilala maeneo ya wazi, 200 kati ya wahamiaji hao ni watoto ambapo IOM, UNHCR na shirika la Save the Children wamejitahidi kuwapatia malazi.