Usawa wa kijinsia vijijini unaimarika:UM

8 Februari 2011

Umoja wa Mataifa umesema leo kuwa umefanikiwa kuinua hali ya usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake wengi kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji kwenye sekta ya kilimo katika maeneo ya vijijini, lakini hata hivyo umesema kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili wanawake hao wafaidike na mavuno ya kazi zao .

Katika taarifa yake ya tathmini juu ya hatua zilizofikiwa hadi sasa, mfuko maalumu wa Umoja huo wa mataifa wa kusaidia maendeleo ya kilimo (IFAD) umesema kuwa wanawake wengi sasa wanafursa ya kumiliki rasilimali, kufanya maamuzi na hata kupunguziwa mzigo mkubwa wa kazi kufutia kuimarika kwa huduma za kijamii ikiwemo pia miundo mbinu jambo ambalo linatia moyo na kuleta sura mpya.

IFAD imesisitiza kuwa imedhamiria kuendelea kuweka msukumo wake kwenye maeneo ya vijijini ambako idadi kubwa ya wananchi wake hasa wanawake bado wanakabiliwa na hali ya umaskini mkubwa.  Kupitia mafanikio hayo yaliyoanza kujitokeza IFAD inakusudia kuzidisha kazi kuhakikisha kwamba kundi kubwa la wanawake wanaanza kufaidika na matunda yatokanayo ya jasho lao.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud